Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) – ABNA –, Ayatollah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wa mnasaba wa kuuawa Shahidi Mujahid Mkubwa na Mshika Bendera wa Mapambano ya Muqawamah, Hojjat al-Islam Sayyid Hassan Nasrullah, sanjari na kutoa pongezi na salama za rambirambi za kuuawa Shahidi Kiongozi huyo wa kipekee wa Hezbollah kwa safu nzima ya Muqawamah na Umma wa Kiislamu, na kutangaza siku tano (5) za maombolezo ya umma nchini humo, amesisitiza akisema:
Msingi aliouanzisha (na kuusimika) huko Lebanon na katika vituo vingine vya nguvu (za Muqawamah), ametoa mwelekeo. Kwa kumpoteza Sayyid Mpendwa, sio tu kwamba Upinzani (Muqawamah) hautatoweka, bali pia utapata nguvu (na uimara) zaidi kwa baraka ya damu yake na Mashahidi wengine wa tukio hili, na mashambulio ya safu ya Muqawamah (Upinzani) dhidi ya mwili uliochakaa na kuoza wa utawala wa Kizayuni yatakuwa ya kuumiza (na makali) zaidi.
Andiko la ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi ni kama ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Hakika Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na Kwake Tutarejea
Wapendwa watu wa Iran
Ummah Mkubwa wa Kiislam
Mujahid Mkubwa, Mshika Bendera wa Upinzani katika eneo, Mwanazuoni Mwenye Maadili ya Kidini na Kiongozi wa Kisiasa Mwenye Busara, Mpendwa Sayyid Hassan Nasrullah Mwenyezi Mungu awe radhi naye, alikufa Shahidi katika matukio ya jana usiku huko Lebanon na akaruka na kuelekea katika Ulimwengu wa juu zaidi (Ulimwengu wa Malaika).
Sayyid Mpendwa, alipata (thawabu) malipo ya miongo kadhaa ya Jihad katika Njia ya Mwenyezi Mungu na kukakibiliana na misukosuko yake wakati wa mapambano matakatifu.
Aliuawa Shahidi wakati akijishughulisha na mipango ya kuwalinda watu wasio na makazi (waliofurushwa katika nyumba zao) wa vitongoji vya Beirut na nyumba zao zilizoharibiwa na wapendwa wao (waliokimbia nyumba zao na kuenea maeneo ya wazi), kama vile alivyokuwa pia akipanga mipango ya mapambano na jihadi kwa miongo kadhaa kwa ajili kuwatetea na kuwahami watu wanaodhulumiwa wa Palestina na miji na vijiji vyake vinavyokaliwa kwa mabavu, na nyumba zao zilizoharibiwa, na wapendwa wao waliouawa kwa umati. Neema hii ya kufa Kishahidi baada ya mapambano na jihadi zote hizo, kwa hakika ni haki yake isiyopingika.
Ulimwengu wa Kiislamu, Shakhsia zenye adhama kubwa; na safu ya Muqawamah (Upinzani) ambayo ni mshika bendera wa viwango bora, na Hezbollah ya Lebanon, wamempoteza Kiongozi bora asiye na kifani, lakini baraka ya mipango na Jihad yake ya miongo kadhaa, haitapotea kamwe. Msingi aliouanzisha (na kuusimika) nchini Lebanon, na kutoa mwelekeo kwa vituo vingine vya upinzani, kwa kumpoteza yeye si tu kwamba hautatoweka, bali pia utazidi kupata nguvu (na uimara) zaidi kutokana na baraka ya damu yake na Mashahidi wengine wa tukio hili.
Mashambulio ya safu ya Muqawamah (Upinzani) dhidi ya mwili uliochakaa na kuoza wa utawala wa Kizayuni yatazidi kushtadi zaidi. Dhati mbaya (na iliyochafuka) ya utawala wa Kizayuni haijashinda (haijapata ushindi wowote) katika tukio hili.
Sayyid wa Upinzani hakuwa ni mtu tu, bali pia alikuwa ni njia na ni shule, na njia hii itaendelea kama ilivyo. Damu ya Shahidi Sayyid Abbas Mousawi haikukaa (na kuishia) ardhini (tu), na hivyo hivyo damu ya Shahidi Sayyid Hassan haitakaa ardhini.
Natoa pongezi na salam zangu za rambirambi kwa Mke Mpendwa wa Sayyid Mpendwa, ambaye pia alitangulia kumtoa mwanawe ‘Sayyid Hadi’ katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na kwa Watoto wake na kwa familia za Mashahidi wa tukio hili, kwa kila Mwanachama wa Hezbullah, kwa watu wote wapendwa na viongozi wa ngazi za juu wa Lebanon, na kwa pande zote za safu ya Upinzani (Muqawamah), na kwa Umma wote wa Kiislamu kwa kuuawa ‘Shahidi Nasrullah’ Kiongozi Mkuu na Masahaba zake waliouawa kishahidi pamoja naye, na ninatangaza rasmi siku tano za maombolezo ya ummah katika nchi nzima ya Iran ya Kiislamu. Mwenyezi Mungu awawafufue Mashahidi hawa pamoja na Mawalii wake.
Na amani iwe juu ya Waja wa Mwenyezi Mungu waliowema.
Sayyid Ali Khamenei
28 Septemba, 2024.